← Rudi MaktabaniPakua PDF ya Asili

TANZANIA ASSEMBLIES OF GOD

TAMKO LA KUJIWEKA WAKFU KWA AJILI YA MIAKA 13 YA MOTO WA UAMSHO

THE SEASON OF REVIVAL FIRE

2020–2033

UTANGULIZI WA TAMKO

Kwa kuwa TUNAAMINI kuwa huu ni wakati wa uamsho, yaani kurudiwa kwa Pentekoste ndani ya Kanisa (Matendo 2:1–4; 4:31);

Kwa kuwa TUNAAMINI juu ya yale yaliyotokea katika huduma ya Bwana wetu Yesu Kristo na katika kanisa la Matendo ya Mitume (Matendo 10:38–40), na ya kuwa tukiomba na kuvuviwa matendo hayo yaweza kutokea leo (Yohana 14:12);

Kwa kuwa TUNAAMINI kuwa tamko la Halmashauri Kuu ya TAG lililopitishwa na Baraza la Waangalizi na kisha kuthibitishwa na Baraza Kuu kupitia konferensi za majimbo yote sabini na moja (71), kwamba miaka hii kumi na tatu (13) ya 2020–2033 na kuendelea, kuwa ni miaka ya moto wa uamsho ya kumtaka Bwana na NGUVU ZAKE.

Kwa kuwa TUNAAMINI kuwa tumeisikia vema sauti ya Roho Mtakatifu ikiongea na mioyo yetu kama kanisa la nchi lenye maono makubwa;

Sisi kanisa la Tanzania Assemblies of God, tunatamka tamko la kujiweka WAKFU kwa Bwana na UWEZA wa NGUVU ZAKE kama ifuatavyo:

SEHEMU YA KWANZA: TAMKO LA KUJIWEKA WAKFU

1. Kujiweka Wakfu kwa Maombi na Uamsho

TUNAJIWEKA WAKFU kufunga na kuomba, kuimarisha ushirika na umoja wa kanisa na kuendelea kuhubiri mahubiri ya Kipentekoste tukitazama umwagiko wa Roho Mtakatifu katika nchi yote ya Tanzania na nje ya mipaka yake.

Tukiomba sawasawa na Mambo ya Nyakati wa Pili 7:14 na Habakuki 3:2; kwa ajili ya uamsho mkuu Tanzania unaoambatana na Nguvu za Kipentekoste, na udhihirisho na utendaji kazi wa Roho Mtakatifu kwa kiwango cha juu katika kanisa lake (Matendo 1:8).

2. Kujiweka Wakfu Kutimiza Agizo Kuu

TUNAJIWEKA WAKFU SISI WENYEWE kwa makusudi kabisa kutimiza AGIZO KUU ambalo linatutuma kuhubiri habari njema (Yesu anaokoa, Yesu anaponya, Yesu anajaza Roho Mtakatifu na Yesu anarudi tena) ulimwenguni kote na kwa kila kiumbe kwa kutumia mbinu mbalimbali (Mathayo 28:19).

Tunaunganisha nguvu zetu katika taifa zima kama kanisa, pamoja na washirika wenza ndani na nje ya nchi, watakaosimama katika kuwasha moto wa Roho Mtakatifu na hivyo kumletea Mungu mavuno makubwa.

3. Wito kwa Watumishi na Washirika Wote

TUNAWAITA WATUMISHI NA WASHIRIKA WOTE wa TAG kujitoa dhabihu na kuonesha uzima mpya, nguvu mpya na uhai mpya kwa maombi, mifungo na mikesha (Waefeso 6:18; Matendo 2:17–18); kujenga ushirika na umoja wa kanisa; malezi ya waongofu wapya na mafunzo kwa washirika; kuanzisha na kuimarisha huduma za watoto, vijana na wanafunzi; kuanzisha na kutumia kwa utukufu wa Mungu vikundi vya sanaa na michezo; na kuanzisha na kutumia miradi inayoonesha upendo wa Yesu Kristo kwa jamii.

SEHEMU YA PILI: MALENGO YA MIAKA 13 YA MOTO WA UAMSHO

TUNAAMINI kwa uweza wa Mungu, kwa umoja na kwa pamoja, tutatenda MAKUU hadi kufikia malengo yafuatayo:

1. Uamsho wa Kiroho Katika Taifa

TUNAMWAMINI MUNGU KUWA NA UAMSHO utakaomwagika nchi nzima na kusababisha mafuriko makubwa ya utendaji wa Roho Mtakatifu kwa kanisa kama matokeo ya kuinua viwango vya maombi yasiyokoma kwa mtu binafsi, makanisani, Sehemu, Jimbo, Idara ngazi zote na Taifa.

2. Uhai na Utendaji Mpya wa Kanisa

TUNAMWAMINI MUNGU KUWA NA UHAI NA UTENDAJI MPYA katika kila kanisa kwa kufanya ibada zenye moto na maadhimisho ya Roho Mtakatifu katika ngazi ya familia, vikundi vidogo vidogo, makanisani na ngazi zote za kanisa.

3. Washirika Milioni Tisa

TUNAMWAMINI MUNGU KUWA NA WASHIRIKA 9,000,000 ifikapo mwaka 2033.

Hii ina maana kila mshirika ni mvunaji na hivyo anawajibika kuleta waongofu wapya wawili au zaidi kila mwaka.

4. Wachungaji Elfu Arobaini na Tano

TUNAMWAMINI MUNGU KUWA NA WACHUNGAJI 45,000 ifikapo mwaka 2033.

Kila Mchungaji azae mchungaji mmoja au zaidi na kumwezesha kusoma chuo cha utumishi kila miaka mitatu.

5. Makanisa Elfu Arobaini

TUNAMWAMINI MUNGU KUWA NA MAKANISA 40,000 ifikapo mwaka 2033.

Kila miaka mitatu, kila kanisa lizae kanisa moja au zaidi na kulitegemeza.

6. Wainjilisti Elfu Nne

TUNAMWAMINI MUNGU KUWA NA WAINJILISTI 4,000 ifikapo mwaka 2033 wanaohubiri katika upako na madhihirisho ya Roho Mtakatifu sawa na Matendo 8:4–25.

7. Wamishenari na Makanisa Nje ya Nchi

TUNAMWAMINI MUNGU KUWA NA WAMISHENARI 200 NJE YA NCHI NA KUFUNGUA MAKANISA 300 ifikapo mwaka 2033.

Kila jimbo liibue, lipeleke na kutegemeza wamishenari wasiopungua wawili (2).

8. Kuzifikia Jamii ambazo Hazijafikiwa na Injili

TUNAMWAMINI MUNGU KUZIFIKIA JAMII 31 za makundi ya watu wasiofikiwa na injili ndani ya nchi kwa njia ya kupanda makanisa ifikapo mwaka 2033.

9. Elimu na Mafunzo ya Watumishi

TUNAMWAMINI MUNGU kuwa na elimu bora na imara na mafunzo kwa watumishi kwa kukamilisha mradi wa kila jimbo kuwa na chuo cha kupanda makanisa, kuendesha mafunzo endelevu, na kujenga na kupanua vyuo mama vya Biblia kufikia udahili wa wanafunzi 3,000 kwa pamoja ifikapo mwaka 2033.

10. Vyombo vya Habari

TUNAMWAMINI MUNGU kuwa na vyombo vya habari vya kanda kama redio na TV na kuwa na chuo cha uandishi wa habari ifikapo mwaka 2033.

11. Miundombinu ya Ofisi za Kanisa

TUNAMWAMINI MUNGU kuwa na ofisi mpya za makao makuu ya kanisa la nchi jijini Dodoma na kila jimbo kuwa na ofisi nzuri ya kisasa jimboni ifikapo mwaka 2033.

12. Teknolojia na Usimamizi wa Rasilimali

TUNAMWAMINI MUNGU kuwa na miundombinu ya kisasa inayotumia teknolojia katika usimamizi wa rasilimali zake zikiwemo fedha, miliki na utawala ifikapo mwaka 2033.

13. Elimu, Shule na Huduma za Afya

TUNAMWAMINI MUNGU kuwa na chuo kikuu kikubwa na bora katika fani mbalimbali, kila kanisa la mahali pamoja, jimbo na idara kuwa na shule ya chekechea, au msingi, au sekondari au vyote kwa pamoja na vituo vya afya ikiwa ni kutimiza wajibu wa kanisa kwa jamii ifikapo mwaka 2033.

14. Kutenda Zaidi ya Tunavyoweza Kufikiri

TUNAMWAMINI MUNGU kufanya zaidi ya yale tunayoweza kuyafikiri na kuwaza kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu (Waefeso 3:20–21).

SEHEMU YA TATU: MISINGI YA UTEKELEZAJI

KWA KUTEKELEZA HAYO:

  • Neno la Mungu ni Mwongozo wetu na mpango wetu wa kazi.
  • Kweli za Kibiblia zisizopotoshwa zitakuwa jumbe zetu za Injili.
  • Roho wa Mungu ndiye mwezeshaji na nguvu yetu ya huduma.
  • Damu ya Bwana Yesu Kristo inatuhakikishia ushindi.
  • Kanisa litakuwa na kuzidishwa kiroho, kiidadi, kijiografia, kiufanisi na kwa wana wapotevu kurudi kwa Bwana Yesu.

KAULI MBIU YETU

“MIAKA KUMI NA TATU YA MOTO WA UAMSHO, TUNAMTAKA BWANA NA NGUVU ZAKE”

“TUNAMTAKA BWANA NA NGUVU ZAKE, MIAKA KUMI NA TATU YA MOTO WA UAMSHO”

“PAMOJA NA BWANA, KWA UMOJA NA KWA PAMOJA, TUTATENDA MAKUU”